Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA –, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Haki za Binadamu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hamid Ahmadi, amesema Tehran na Moscow zimekubaliana kuimarisha mazungumzo yao kuhusu haki za binadamu na kuandaa mtazamo mpya wa pamoja wa kukabiliana na simulizi la Magharibi kuhusu masuala hayo.
Akizungumza akiwa mjini Moscow baada ya kumalizika kwa duru ya 11 ya mazungumzo ya haki za binadamu kati ya Iran na Urusi, Ahmadi alisema pande hizo mbili zilifanya majadiliano yenye tija yaliyolenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja hiyo. Alibainisha kuwa mazungumzo hayo yamekuwa yakiendelea kwa takriban miaka ishirini, licha ya kusimama kwa muda katika vipindi mbalimbali.
Ahmadi alisema pia alikutana na maafisa wa Urusi, akiwemo Kamishna wa Haki za Binadamu wa nchi hiyo, ambapo walijadili athari za kibinadamu na kisheria zilizotokana na mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wananchi wake.
Kwa mujibu wa Ahmadi, Iran na Urusi zimekubaliana kuwasilisha mtazamo mpya wa haki za binadamu unaotokana na misingi ya ustaarabu wao, kama mbadala wa simulizi wanalosema ni la upande mmoja linalotolewa na nchi za Magharibi.
Aidha, alieleza kuwa alishiriki katika mkutano uliofanyika katika Chuo cha Urusi cha Uchumi wa Taifa na Utumishi wa Umma chini ya Ofisi ya Rais wa Shirikisho la Urusi, ambapo washiriki walijadili nafasi ya teknolojia za kisasa, hususan akili bandia (AI), na athari zake kwa haki za binadamu.
Maoni yako